Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni
Naibu Waziri Sayansi na Teknolojia, January Makamba akipokelewa na akina
mama na kupewa baraka zake.
...Wananchi wakimsikiliza.
Wakazi mbalimbali wa Jimbo la Bumbuli,
wilayani Lushoto, Mkoani Tanga wamesema kuwa wapo tayari kumuunga mkono
Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba kama ataamua kuwania nafasi ya
kuwa mgombea wa Uraisi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wakazi hao ambao walionyesha nia yao hiyo
katika sehemu mbalimbali alizopita Mbunge huyo katika ziara yake ya siku
sita kutembelea jimbo lake iliyoanza Machi 30. Makamba ni mmojawapo wa
watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya Urais.
Alipokuwa katika kata ya Tamota, viongozi
wa dini walimfanyia maombi maalum ambayo yaliongozwa na Mchungaji
Amasia Mweta na Sheikh Amiri Yahaya Shekibula mara baada ya kumalizika
kwa mkutano wa hadhara uliohutumbiwa na Mbunge huyo kijana.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Bumbuli
katika maeneo yote aliyopita kwenye ziara yake, Makamba aliwashukuru
wakazi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa Mbunge wao na kusema kama sio
wao asingeweza kuonekana na kutajwa katika kuwania nafasi ya kuwa
mgombea wa CCM.
Makamba, huku akishangiliwa na wakazi hao
wa maeneo hayo, alisema kuwa hakuna namna ambayo unaweza kutengeneza
watu kukutaja katika nafasi za juu bila kupitia kwa wananchi kukuchagua
katika nafasi ya kuwawakilisha.
“Kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za
uchaguzi sio sumu si dhambi pia kuchukua na kuingia katika
kinyang’anyiro hicho,” alisema na kuongeza kuwa sasa hivi kuna kiu kubwa
ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemuona na kumtaja yeye jambo
ambalo si baya.
Nao wananchi , wakiwemo vijana, kina mama
na wazee katika maeneo mbalimbali aliyopitia Makamba, walimhakikishia
Mbunge huyo kuwa hivi sasa hawatampokea mtu yeyote ambaye atakuja
kujipitisha katika jimbo hilo hadi hapo watakapojua hatma ya utekelezaji
wa nia ya Mbunge huyo kuwania nafasi ya kuwa mgombea wa Urais kupitia
CCM.
Nao waumini wa Usharika wa Bumbuli
walimtaja Mbunge huyo kuwa jasiri, mweledi na mwenye maono mapana na
wakasema wanaahidi kuwa bega kwa bega katika harakati hiyo ya kuwania
kuwa mgombea wa CCM.
No comments:
Post a Comment