Mfumo Mpya Wa Bima Ya Afya Ya Kinga Ya Waendesha Bodaboda Yazinduliwa

Mkuu wa Kitengo cha Elimu na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ACP Abel Swai (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Nje wa Vodacom Rosalynn Mworia (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi wa bima ya waendesha pikipiki (bodaboda) iliyofanyika katika viwanja vya TCC Chang’ombe jijini. Hafla hiyo ya uzinduzi ilidhaminiwa na Vodacom Tanzania.



Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Nje wa Vodacom Rosalynn Mworia (wa kwanza kushoto) akimkabidhi sare za waendesha pikipiki (bodaboda) Katibu wa Chama cha Waendesha Pikipiki Mkoa wa Kipolisi wa Temeke Bakari Sangalla (wa tatu kutoka kushoto) baada ya uzinduzi wa bima ya ajali na sare za utambulisho wa waendesha pikipiki mkoani Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jumanne Manji (wa pili kutoka kushoto). Hafla hiyo ilifanyika viwanja vya TCC Chang’ombe jijini.
Baadhi ya madereva wa bodaboda wakimsikiliza kwa makini mshereheshaji  na mtangazi wa kituo cha Clouds Radio Frank Kibonde  wakati wa  hafla ya uzinduzi wa huduma za bima ya waendesha bodaboda na sare za utambulisho katika viwanja vya TTC Chang’ombe jijini chini ya udhamini wa Vodacom Tanzania.
Wanamuziki wa bendi ya Yamoto wakitoa  burudani kwa  waendesha bodaboda na wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla hiyo ya uzinduzi bima kwa madereva wa bodaboda na sare za utambulisho ambayo imeanzishwa kwa ushirikiano wa makampuni ya Vodacom Tanzania na Alternative Solutions iliyofanyika katika viwanja vya TTC Chang’ombe.
.Idadi kubwa ya pikipiki zikiwa zimeegeshwa  viwanja vya TCC Chang’ombe.Pamoja na mgomo wa mabasi ya kubeba abiria unaoendelea jijini waendesha bodaboda waliacha kwa muda kazi ya kubeba abiria na kuhudhuria kwa wingi katika hafla hiyo ya uzinduzi wa bima kwa ajili yao ambayo imeanzishwa kwa ushirikiano wa makampuni ya Vodacom Tanzania na Alternative Solutions
Waendesha pikipiki maarufu kwa jina la Boda boda hivi sasa wanaweza kupata huduma za matibabu wanapopata ajali za barabarani.Hii ni kutokana na  kuzinduliwa kwa bima inayowalenga ambayo imeanzishwa kwa ushirikiano wa makampuni ya Vodacom Tanzania na Alternative Communications.Waendesha bodaboda  wapatao 750 kwa kuanzia kutoka wilaya za Ilala,Temeke na Kinondoni watakuwa wanufaika wa  huduma hii ambayo imezinduliwa jijini Dar es Salaam
Uzinduzi huu umefanyika leo  na mgeni wa heshima alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Saddick na ulihudhuriwa na waendesha bodaboda,maofisa wa serikali,na askari wa kikosi cha usalama barabarani ambapo waendesha  bodaboda walikabidhiwa vifaa vya kuwakinga wakati wa ajali na sare maalum za kuwatambulisha wanapokuwa kazini
Waendesha bodaboda watakaokuwa kwenye mpango huu muda wote watatakiwa kuwa wamevaa sare zilizoandikwa namba zao maalum za kuwatambulisha,kituo wanachoegesha  pikipiki zao na namba maalumu ya kupiga wakati wakati wa dharura.
 Waendesha bodaboda wataweza kuingia kwenye mpango huu wa bima ya kuwakinga na kupatiwa sare pindi watakapofuata utaratibu uliowekwa wa kujiunga kwa mujibu wa kanuni za  kufanya biashara ya kuendesha pikipiki za wilaya wanazofanyia kazi.
Huduma hii imebuniwa kutokana na ongezeko la ajali za pikipiki na pia biashara hiyo kuhusishwa na vitendo vya uharifu mara kwa mara.Sare zitasaidia abiria kuwatambua  waendesha bodaboda halisi wanaopaswa kuwakodisha na bima ya afya itawasaidia wakati wa majamnga ya ajali na kupoteza maisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Alternative Communication Edward Mgaya alisema “bima hii mpya iliyozinduliwa leo itawawezesha waendesha bodaboda kupata huduma za matibabu wakati wanapopatwa ajali au kulipa mafao familia zao wakati mhusika aliyekata bima anapopoteza maisha.Mchango wa bima hii kwa mwezi ni shilingi 3,000/- ambapo mwendesha bodaboda atakayejiunga na mpango huu atatakiwa kulipia shilingi 1,000/-ambapo fedha zinazoongezeka  zitalipwa kwa ruzuku maalumu
Alisema waendesha bodaboda watakaojiunga na mpango huu ni lazima kutumia vifaa vya kuwakinga vilivyotolewa ikiwemo kuvaa sare ili wapatapo ajali waweze kulipwa kwa mujibu wa taratibu za bima hii.
Akiongea kwa niaba ya Chama cha Waendesha Bodaboda,Bwana Bakari Sagalla aliipongeza Vodacom na Alternative Communication kwa kuja na ubunifu huu ambao umelenga kuwakinga  waendesha bodaboda nchini  kimaisha na kusaidia biashara hii kuwa na mpangilio maalumu tofauti na hivi sasa.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza alisema “Tunaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali kutoa elimu ya usalama barabarani kwa jamii ya watanzania.Ushirikiano huu na kampuni ya Alternative Communication ni ubunifu wenye tija ambao utapunguza ajali za pikipiki na vitendo vya uharifu kutumia vyombo hivi”
Sare maalumun zilizotolewa zitawatofautisha waendesha bodabado halisi na wale wanaotumia kisingizio cha kubeba abiria na kujihusisha na vitendo vya uharifu.
Ushirikiano huu pia utatoa fursa kwa waendesha bodaboda watakaotaka kufanya biashara ya M-Pesa katika maeneo wanayofanyia kazi au kuitangaza huduma hiyo na watajengewa mazingira bora ya kufanya biashara hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadick  ambaye alikuwa mgeni rasmi aliipongeza Vodacom na   Alternative Communication kwa kuja na ubunifu huu muhumi wenye lengo la kupunguza ajali za pikipiki na kuboresha maisha ya waendesha vyombo hivyo na alizitaka taasisi nyingine na makampuni kuiga mfano huu na kuingia kwenye kampeni hii.
 Mkuu wa Kitengo cha Elimu na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ACP Abel Swai  alisema kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikiongezeka na kusababisha vifo na ulemavu kwa wananachi wengi.Alisema ajali za bodaboda nyingi zinachangiwa na waendeshaji wake kutofuata sheria zan usalama barabarani na uzembe na aliwahimiza waendesha bodaboda kuchangamkia fursa ya mpango huu wa bima ambapo wataweza kupata  vifaa vya kinga,bima na elimu ya usalama barabarani.
 Baada ya  mpango huu kuzinduliwa Dar es Salaam utafuatia mkoa wa mbeya na mikoa mingine nchini.Vodacom imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali za kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia kampeni yake ya ‘Wait to Send’ inayowahamasisha madereva kutotumia simu wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto.

No comments:

Post a Comment