AFISA CHUO KIKUU MIKONONI MWA KOVA KWA MAUAJI


Afisa Mwandamizi Idara ya Utawala wa Chuo Kikuu Huria jijini Dar es Salaam aliyetambulika kwa jina la Brown Ng’ingo (pichani) amejikuta mikononi mwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar, Kamishna Suleiman Kova baada ya kudaiwa kumtishia kumuua mwanamke aliyekuwa akiishi naye.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni katika ofisi zetu, mama huyo aliyemfikisha afisa huyo kwa Kamishna Kova aliyejitambulisha kwa jina la  Enjoi Belege, alisema alichukua hatua hiyo baada ya kuona maisha yake yako hatarini kutokana na vitisho vya mwanaume huyo.
Aidha, mama huyo anadai kuwa wakati wanakutana na ofisa huyo kwa mara ya kwanza alimwambia  hakuwa na mke jambo aliloliona ni sahihi kuishi naye kuliko kuendelea kukaa peke yake.Akisimulia mkasa huo mama huyo alikuwa na haya ya kusema:
“Awali nilikuwa na mwanaume naishi naye lakini alikuwa ni mtu kutoka nje, alipewa notisi ya kuondoka nchini kwa saa 24 na serikali, akaondoka.“Baada ya kuondoka nikaa peke yangu bila mwanaume, hivyo baada ya kukutana na huyu  mwanaume nilijisikia faraja kubwa.
“Lakini baada ya kukaa kwa muda fulani hali ilibadilika akaanza kunipa vipigo na manyanyaso siku hadi siku ikiwa ni pamoja na kunitishia kuniua kwa kutumia kisu.“Siku moja alitaka kuninyonga shingo hali iliyonifanya nikimbilie  Kituo cha Polisi Kawe wakamfungulia jalada namba KW/RB/1128/2015 KUTISHIA KUUA KWA KISU.
“Kitendo cha kuninyonga kilinifanya nikae nyumbani nikiwa ninaumwa pia bila kufanya kazi yoyote ile.”
Alidai kuwa pamoja na kumfungulia kesi polisi Kawe lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na askari wa kituo hicho huku vitisho kutoka kwa mwanaume huyo vikiendelea.
“Kutokana na kukosa amani na uwoga wa kuuawa, nikaamua kwenda kwa Kamishna Kova kumuomba msaada zaidi kwani alikuwa akinitumia sms (ujumbe) wa vitisho.“Pale Kova alinikabidhi wasaidizi wake ambao walifungua jalada lenye kumbukumbu namba CD/RB/4823/2015 na CD/IR/1160/2015 KUTISHIA KUUA KWA MTANDAO 9/4/2015.”
Aliongeza kuwa Kova alifanikisha kumtia nguvuni mwanaume huyo.
Waandishi wetu walimtafuta Ng’ingo na aliposomewa madai hayo alisema anamfahamu huyo mwanamke.
Akaongeza:  “Huyo dada sijawahi kuwa na husiano naye japokuwa namfahamu, nilimchukua tu anisaidie kumuuguza mgonjwa wangu nyumbani kwangu, sasa nashangaa hayo yote yanatoka wapi?”
Alipoulizwa kuhusu kufunguliwa mashitaka polisi na mama huyo, hakujibu, alikata simu.

No comments:

Post a Comment