ADAIWA KUBANJUKA NA AUNT, BAADAE ALIAMUA KUJITOSA KWA LULU - 7


JUMAMOSI iliyopita tuliishia pale nguli wa sinema za Kibongo, hayati Steven Kanumba alipoanzisha uhusiano wa kimapenzi na mrembo aliyetwaa taji la Miss Kinondoni, Sylvia Shally.
SASA ENDELEA...
Walipendana sana, kama ilivyokuwa kwa wapenzi wake waliotangulia, vyombo vya habari vilianza kuwafuatilia lakini wenyewe hawakujali. Walipendana sana. Kwa kipindi cha mwaka mmoja waliishi kama bibi na bwana.Baadaye nao walianza kugombana mara kwa mara. Maisha yao yalimulikwa kila wakati na vyombo vya habari.
Kuna wakati Kanumba alikwenda Marekani, Sylvia alibaki nyumbani Tanzania. Kipindi hicho vyombo vya habari vilizidi kueneza habari za kutatanisha kuhusu uhusiano wao. Kuna wengine walisema wameshamwagana lakini wengine wakasema bado.Lakini kama ilivyokuwa kwa Wema na Nargis, ilifika wakati Sylvia na Kanumba nao wakamwagana.
AKOMAA
NA FILAMU
Kazi na dawa, baada ya kuachana na mrembo huyo, Kanumba alielekeza nguvu zake katika kurekodi sinema. Akatoa sinema kama Fake Smile, Unfortunate Love ambayo aliigiza na wakali kama Aunt Ezekiel, Lisa Jensen na Zamda Salum.
Sinema hiyo ilikuwa gumzo kutokana na kuzungumzia jinsi gani mtu unaweza kumtamani mtu ndani ya dakika moja, inahitaji saa nzima kumpenda mtu, inahitaji siku nzima kumuenzi mtu lakini inahitaji maisha kutomsahau mtu.
Baada ya muvi hiyo akatoa, Hero of The Church ambayo ilikuwa na mafundisho ya dini. Kanumba akiwa kama mhusika mkuu, alionesha anapambana na wazee wanaowadanganya waumini na kufichua ukweli wa mambo.
Mwendo wa kurekodi sinema ukaendelea, akatoa Saturday Morning, Crazy Love, More Than Pain, Uncle JJ, This is It, Off Side, Deception, Young Billionaire na Devil Kingdom ambayo ameigiza na mwigizaji mkali kutoka Nigeria, Ramsey Nouah.
Filamu hiyo imeonesha uwezo wa nguvu za shetani. Nguvu ya giza ilitumika kushawishi watu waamini muujiza wa Mungu lakini mwisho wa siku ukweli ulijulikana kwamba Mungu anabaki kuwa Mungu na ndiye anayeweza yote.
ADAIWA KUBANJUKA NA AUNT EZEKIEL
Wakati akiendelea kufyatua sinema, Steven alidaiwa kuanzisha uhusiano wa siri na muigizaji Aunt Ezekiel. Uhusiano huo ulifichwa sana na hata vyombo vya habari havikuweza kuambulia.
AJITOSA KWA LULU
Mwaka 2012, uhusiano wa Aunt na Kanumba haukudumu sana, akahamishia majeshi kwa mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18.Kama ilivyokuwa kwa Aunt, uhusiano wa Lulu na Kanumba nao ulikuwa wa siri.
Vyombo vya habari havikuwa na la kusema hadi siku ya kifo cha Kanumba. Lulu akakiri kuwa walikuwa wapenzi baada ya tukio hilo na walikuwa chumbani pamoja wakati wa kifo chake.
Vyombo vya habari vikaanza sasa kuripoti mambo mbalimbali yaliyokuwa yamejificha kati ya wawili hao. Mwigizaji huyo alifunguliwa mashtaka ya kuua bila kukusudia ambapo kesi inaendelea hadi sasa.

No comments:

Post a Comment