JIFUNZE KUKUBALI UNAPOKOSEA USIMWUMIZE MPENZI WAKO

Makosa tumeumbiwa binadamu ni kweli! Ila si kukosea kwa makusudi na kukataa kwa nguvu. Hiyo inakera na inaudhi sana kwa wapenzi. Kukubali kosa siyo vibaya wala haimaanishi kwamba umeonesha udhaifu hapana bali utakuwa umetengeneza mazingira mazuri ya kujua namna ya kuishi na mpenzi wako.
Nasikitika kusema kuwa wapenzi wengi wa sasa wamekuwa na tabia ya ugumu wa kuukubali ukweli pindi wanapowakosea wapenzi wao.
Jambo hilo husababisha upande mmoja kuishi kwa unyonge katika uhusiano wao kwa sababu ya kuona ananyanyaswa kimapenzi na kujikuta kisaiklojia akijenga kitu kichwani mwake kuwa wewe unamfanyia hivyo kwa sababu ya mazingira mliyokutana. Labda kwa sababu unajua wazazi wake walishafariki dunia au mlipo na kwao ni mbali na hana fedha ya kumfikisha huko.
Hali hiyo humfanya mpenzi wako kujiona mnyonge, mpweke, asiye na nguvu kwa sababu tu labda anakupenda kupita kiasi au mmetoka mbali kimapenzi au mlioana kwa nguvu na ujanjaujanja bila baraka za wazazi.
Ninachoamini, kama umekosea, hata kama utajifanya kukataa kwa macho ya kawaida ila kwa ulimwengu wa roho, nafsi yako itakusuta tu, hasa ukikaa peke yako na kuanza kurudia matukio yako katika siku husika (review)
Pengine umefanya hivyo kwa sababu ya mfumo dume ulionao kwa mpenzi wako au umefanya hivyo kwa sababu wewe mwanamke ndiye unayemuweka mjini mwanaume.
Hebu kubali kutoka moyoni kama kweli umekosea, haiwezekani mwanadamu ukawa hukosei. Endapo utakuwa na tabia ya kuukubali ukweli pindi unapokosea ni dhahiri utaweza kujifunza vitu vingi katika maisha kutokana na makosa.
Zipo faida nyingi za kuukubali ukweli unapokosea. Kwanza ni kujifunza kuwa kile ulichomfanyia mwenzi wako kinamuudhi. Pili, uhusiano wenu utaendelea kudumu kwa sababu chanzo cha migogoro umekitambua.
Tatu, hata wewe utakuwa mwalimu na shuhuda kwa wapenzi wengine wenye ubishi na tabia kama zako.
Kwa wapenzi inachukiza sana kuona kila siku mpenzi wako anakosea kosa lilelile ambalo jana, juzi na wiki kadhaa amekuwa akilitenda. Hii inaumiza sana, ni heri ukafanya kosa lingine jipya bila kujua kuliko kufanya kosa lilelile kila siku, inakera!
Tukutane wiki ijayo kwa nyingine murua ya kujenga uhusiano wako.

No comments:

Post a Comment