KUWA MAKINI KATIKA KUWASHAURI WAPENZI

Kama unataka kuwashauri watu walio na malumbano katika uhusiano wa mapenzi basi kwanza washauri kwa kuutenga ukweli na uongo bila kuegemea upande mmoja. Pili kuwa makini kuuponda upande mmoja ambao haupo karibu yako wakati ukimshauri mwenza wake.
Kama upande usiokuwepo ukija kusikia kuwa uliuponda unaweza kudhani ulifanya hivyo kwa sababu una masilahi yako binafsi kwa mwenza wake au inawezekana unamtaka mwenza wake na ulifanya hivyo ili kuzidi kumnyong’onyesha yeye huku wewe ukijitengenezea mazingira ya ushindi kwa kutumia ugomvi wao.
Kwa wapenzi unaowashauri, kuna mawili baada ya ushauri wako, inawezekana ukawa umetibu tatizo lao na wao kujijenga vizuri katika uhusiano au ushauri wako ukabomoa kabisa  uhusiano wao.Kama utafanikiwa kuujenga na kuuimarisha uhusiano wao kwa maneno yako ni jambo jema ambalo siku zote wao watajivunia kama wapenzi, lakini pia hata wewe itakuwa ni furaha maishani mwako kuona wapendanao au ndoa ya f’lani ikiendelea kudumu kwa sababu ya ushauri wako.
Lakini kama ushauri wako utasababisha kuvunja uhusiano au ndoa ya wawili wale ni dhahiri, mmoja wapo atajenga chuki na wewe kwa kuamini kuwa ulichangia kwa asilimia kubwa kuvunjika kwa uhusiano wao.
Linapokuja suala la kuwashauri wapenzi walio kwenye mgongano au wameachana unapaswa umshauri kuwa makini sana la sivyo unaweza kujiingiza kwenye mgogoro usio kuhusu.Simaanishi usiwashauri ila jaribu kuwa makini usije ukaegemea upande mmoja, kama utashauri basi simama kwenye ukweli bila kumtetea mtu wa jinsi yako kama amekosa, kama utamtetea basi utakuwa haujawasaidia kitu zaidi ya kumpa kichwa aliyekosea na kujiona yuko sawa.
Endapo aliyekosea akibaini kuwa ulikuwa unamkandamiza kwa kumtetea mtu wa jinsi yako, atachukia na kuamini watu wa jinsi ile wote hawana maana na kumfanya atengeneze fundo la chuki moyoni mwake.
Tukutane wiki ijayo katika mada nyingine nzuri zaidi.

No comments:

Post a Comment