HATA UMPE NINI, KAMA HAKUPENDI, HAKUPENDI TU ACHANA NAYE

Wiki iliyopita nilianza kuzungumzia juu ya mada yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu. Ni mada ambayo nadiriki kuiandika kwa kirefu ili wale ambao wana ulimbukeni wa kutaka kulazimisha kupendwa kwa kutoa vitu, wajue wanakosea na penzi wanalotafuta kwa njia hiyo ni lile lililooza.

Kwa nini nimeamua kuandika mada hii? Kwanza ni kile ambacho nimekuwa nikikiona kwenye jamii ninayoishi. Watu kupenda kulazimisha penzi na kuwa tayari kufanya lolote ili wapendwe.
Hilo ni tatizo na ndiyo maana nikaona nitumie kalamu yangu kuwaelimisha watu hao. Pili ni ushuhuda wa mmoja wa wasomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina moja la Nadhifa, mkazi wa Arusha ambaye alinipa kisa cha kusikitisha.
Huyu ni msichana ambaye anatokea kwenye familia yenye uwezo kifedha lakini alichokuwa anakikosa ni penzi la kweli kutoka kwa mwanaume aliyempenda.
Kwa maelezo yake anadai alitokea kumpenda kijana mmoja ambaye aliamini huyo ndiye mume wa maisha yake.
Alichokosea sasa ni kwamba, baada ya kujua kwamba analo penzi la dhati kwa mwanaume ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alianza kumpa zawadi za hapa na pale, wakati mwingine pesa.
Mwanaume naye kama walivyo wanaume wengi wa mjini kupenda mteremko, alipobaini kuwa binti huyo kamzimia, akawa anamkubalia kuwa na yeye anampenda kumbe ni usanii mtupu.Basi binti wa watu akajiaminisha kuwa amepata mwanaume, akajiachia. Alichokuwa akifanya Nadhifa ni kuhakikisha kila anachohitaji mwanaume huyo anampatia.
Akakosea sana pale mwanaume huyo alipomtaka ampe mapenzi kinyume na maumbile na kumkubalia akijua ni njia ya kumshika.Hapo ndipo alipoharibu na kwa kuwa mwanaume yule alikuwa hana mapenzi ya kweli, akaanza kumfanyia kila aina ya vituko. Si alijua hawezi kuachwa? Kwa hiyo mpaka sasa uhusiano wao upo upo tu.
Binti wa watu bado anajitahidi kuonesha upendo lakini mwanaume anamzuga, yaani haoneshi kwamba anampenda kwa dhati.
Mpenzi msomaji wangu, hili ni kosa ambalo watu wengi wanalifanya. Tunatumia nguvu kubwa hata kufanya yasiyostahili eti ili kuwapata na kuwashika wale ambao tumetokea kuwapenda.Ukweli ni kwamba, anayekupenda wala huwezi kutumia nguvu kubwa kumpata wala kumshawishi asikuache. Mwanamke huwezi kumzuia mpenzi wako asikuache kwa kumpa mapenzi kinyume na maumbile. Huko ni kujidhalilisha na kujishusha thamani.
Lakini pia mwanamke huwezi kumpata mwanaume kwa kumhonga hata kama pesa unazo. Ukimwekea chambo ya pesa, kumpa vitu vya thamani eti ili kumfanya akupende, utageuka kuwa mtumwa wa mapenzi na wala usiipate furaha unayoihitaji.
Lakini pia kwa wewe mwanaume ujue kwamba, huwezi kumpata mwanamke na kumshika asikuache kwa kumpa pesa au vitu vya thamani, ukifanya hivyo ujue penzi lenu limeshikiliwa na pesa na kwa kuwa pesa haina thamani kubwa kuliko penzi la kweli, huyo uliyenaye akimpata anayempenda, atakuacha hata kama una pesa zako.
Kikubwa unachotakiwa kukifanya ni kueleza hisia zako na kuonesha wazi kwamba unachokisema kinatoka moyoni mwako. Baada ya hapo, kuwa tayari kwa lolote, kukubaliwa au kukataliwa. Fanya kila unaloweza kuhakikisha unapata mtu ambaye hata bila kumpa kitu awe tayari kusema anakupenda na iwe hivyo mpaka ndani ya moyo wake.
 Niishie hapo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

No comments:

Post a Comment