HUU NDIO NGO WA MCHAWI ULIOZUA KIZAAZAA!

Dustan Shekidele, Morogoro
NI mshangao! Katika hali isiyotarajiwa, ungo wenye vifaa vya kichawi umekutwa jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mazimbu, Dayosisi ya Morogoro na kuzua kizaazaa kikubwa.
Ungo wenye vifaa vya kichawi ukiwa jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mazimbu, Dayosisi ya Morogoro.
Tukio hilo la aina yake lilijiri saa 12  asubuhi, Jumatano iliyopita katika  eneo hilo lililopo Mtaa wa Boma ‘A’ Kata ya Mazimbu mkoani hapa.
Vitu vilivyokutwa kwenye ungo huo ni damu, pembe, nyembe, shanga, kipande cha gazeti, vitambaa vyeusi na vyekundu.
Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na eneo la tukio walimshutumu mkazi mwenzao (jina tunalo) kwamba, ungo huo ulitoka ndani ya nyumba yake.
Kufuatia kuzipa nguvu shutuma hizo, wananchi hao waliizingira nyumba hiyo ya kifahari iliyopo jirani kabisa na Kanisa la KKKT na kusema maneno ya waziwazi kuhusu imani yao. lli kupata ukweli wa madai ya wananchi hao, mwandishi wetu aliingia ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuzungumza na mmiliki wake huyo ambaye alisema:
Wananchi wakiangalia Ungo wenye vifaa vya kichawi.
“Usiku, kama saa 7 hivi, mbwa wangu walipiga kelele sana. Tulipotoka tukakuta huu ungo ila mwenye ungo hatukumuona. Huenda aligonga kwenye nyumba yangu, akaruka ukuta na kukimbia. Kulipokucha ndiyo tukaamua kuutupa nje.”
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na wananchi hao wakidai mchawi mwenye ungo huo alitoka ndani ya nyumba hiyo.
“Kama ni kweli kwa nini mbwa wake wasimng’ang’anie huyo mwanga? Pia tunajua hii nyumba ina mlinzi kwa nini hakumkamata?” alihoji jirani mmoja.
Jirani mmoja yeye alikwenda mbele zaidi kwa kusema:
“Nakumbuka majira ya saa 12 asubuhi kuna mwenzetu mmoja kamuona mtu akitoka ndani ya nyumba hii na ungo na kuutupa kwenye eneo hili la kanisa kisha akarudi ndani fasta.“Tulipokuja kuangalia ndani ya ungo tukakuta damu, pembe, nyembe, vitambaa vyeusi na vyekundu. Majirani tukaamua kukusanyana na kuja kwenye nyumba hii. Tumekuta geti liko wazi huku milango ya nyumba kubwa ikiwa imefungwa kwa ndani.”
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Kilewa Bohari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ilikuwa kazi kubwa, wananchi waliivamia nyumba ya yule bwana wakidai mwanga yuko ndani. Mimi na baadhi ya wajumbe wangu na wananchi tuliingia kwenye ile nyumba na kusachi.
“Kiukweli hatukumwona mwanga na mwenye nyumba anakiri kuna mwanga alianguka usiku kwenye nyumba yake,” alisema mwenyekiti huyo.Licha ya mwenyekiti huyo kuwasihi wananchi hao kuondoka eneo hilo waligoma wakisisitiza mwanga alikuwemo ndani ya nyumba hiyo.
Kufuatia kizaazaa hicho, uongozi wa mtaa huo uliamua kuita polisi ambao walifika na kuuchoma moto ungo huo na kuwatawanya wananchi.

No comments:

Post a Comment