SHOPPING YA MTOTO WA DIAMOND KUFURU!

KAMA ulishawahi kusikia neno kufuru na ukajua maana yake, basi ndiyo imefanywa na Mwanamuziki Bora wa Afrika Mashariki na Kati, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, baada ya kuteketeza mamilioni ya fedha kwa ajili ya kufanya ‘shopping’ ya nguo na vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na mwanaye ikiwa ni siku chache kabla mpenzi wake, Zarinah Hassani ‘Zari The Boss Lady’ kujifungua.

Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akifanya shopping ya mtoto wake anayetarajiwa kuzaliwa.
KITU CHA DUBAI NA LONDON
Akizungumza na Ijumaa mapema wiki hii, mtu wa karibu wa Diamond anayekuwa naye popote anapokwenda alisema kuwa shopping hiyo aliifanya juzikati huko Dubai na jijini London, Uingereza ambako alikwenda kufanya shoo yake ya Diamonds Are Forever.
Alisema kuwa, akiwa London baada ya shoo, Diamond aliona ni vema akafanya manunuzi hayo kwani hivi karibuni atapata mgeni (malaika) kwenye familia yake.
 KUMBE ALIANZA KITAMBO
Mtu huyo aliendelea kunyetisha kwamba, Diamond alinunua vitu vingi zaidi ya hivyo ambavyo alivipiga picha kwani hata kabla ya kununua huko London tayari kuna baadhi alinunua njiani na kuna siku alinunua vingine jijini Dar.
Alisema kuwa kwa harakaharaka hadi sasa vitu ambavyo Diamond ameshanunua ukivipigia gharama ni zaidi ya Sh. milioni 10 za Kitanzania.‘Diamond Platnumz’ akishika tumbo la Zari.
“Mimi nipo na Diamond karibia kila sehemu anakoenda, nataka kukufahamisha kwamba, hivyo vitu ambayo amevianika ni vichache sana maana tangu siku tunaenda London kuna ‘mazagazaga’ kibao alinunua njiani.
“Ukiachia mbali hivyo vitu ambavyo mimi nimevishuhudia kuna vingine vingi,” alisema mtu huyo kwa sharti la kutochorwa gazetini.
 ZARI AANDALIWA BONGE LA PATI
Jamaa huyo aliendelea kutiririka kuwa, pamoja na kutumia mkwanja huo mrefu kwa shopping pia Diamond amejipanga kwa hali na mali kumuangushia Zari bonge la pati inayofahamika kwa jina la Baby Shower ambayo wajawazito wengi huwa wanafanyiwa kabla ya kujifungua na kuzawadiwa baadhi ya mahitaji ya mtoto wa kike atakayezaliwa.

BOFYA HAPA KUMSIKIA DIAMOND
Baada ya kunyetishiwa ishu hiyo, paparazi wetu alifanya mahojiano na Diamond kwa lengo la kutaka kujua gharama za mazagazaga hayo ambayo amenunua kwa ajili ya mwanaye.
Zari akijipiga picha.
Diamond aliweka wazi kwamba kile kitoroli kimoja cha mtoto pekee kilighalimu pauni 1,450 (zaidi ya Sh. 3,625,000).
Alisema kuwa vikorokoro vingine vina thamani ya pauni 1800 (zaidi ya Sh. milioni 4.5) hivyo kwa shopping ya London jumla alitumia pauni 3,250 (zaidi ya Sh. 8,125,000).
Alisema mbali na hivyo kuna vitu vingine ambavyo alivinunua nje ya shopping hiyo hivyo amesahau ni vya aina gani na thamani yake ila kwa harakaharaka hivyo ndivyo anavyokumbuka ingawa thamani inaweza kuwa imepitiliza kwenye Sh. milioni 10 kama kila kitu akikipigia hesabu sawasawa.
“Nafahamu watu wengi wanaweza kushindwa kuamini au kunielewa vizuri ila kweli nimetumia gharama kubwa kununua vitu hivyo ikiwa ni maandalizi ya mwanangu tu.
“Ukweli mimi sitakuwa wa kwanza Tanzania na duniani kununua vitu kama hivyo japokuwa kuna watu wasioacha kubeza wataongea wanachowaza wao,” alisema Diamond.
 WAKOSOAJI WA MAMBO YA WATU
Kwa mujibu wa wakosoaji wa mambo ya watu waliozungumza na gazeti hili baada ya kusikia ishu hiyo walidai kwamba Diamond amefanya kufuru kubwa kwani kuna Watanzania wengi hawana hata fedha ya kununulia kidonge lakini yeye anateketeza mamilioni kwa shopping ambayo hata mtoto bado hajazaliwa.
“Unajua hatuombei litokee jambo baya lakini huyu dogo (Diamond) amefanya kufuru sana maana hata mtoto mwenyewe hajamuona.
“Kibongobongo kuna watu wengi wanasota wanakosa hata mlo mmoja kwa siku lakini yeye anateketeza mamilioni. Ni sawa lakini ajue kuna leo na kesho. Yupo wapi… (anatajwa jamaa mmoja aliyekuwa msanii mkubwa Bongo lakini kwa sasa amefulia).
“Jamaa anatakiwa kuangalia vitu anavyovifanya ili kesho na keshokutwa watu wasisema tulisema..,” alisema mmoja wa wakosoaji hao.
 AGEUZIWA KIBAO
Hata hivyo, wakati mkosoaji huyo akiendelea, mmoja wa Team Diamond aliingilia mazungumzo:
“Acheni hizo, kwa levo ya Diamond lazima afanye hivyo na ukizingatia ni mwanaye wa kwanza. Jamani kwani shopping ya milioni kumi kwa Diamond ni kitu gani? Hivyo ndivyo zinavyokuwa shopping za watoto wa mastaa.
Wewe muone North wa Kanye West na Kim Kardashian anavyofanyiwa shopping ndiyo utajua Diamond ni cha mtoto.”

No comments:

Post a Comment